Featured Post

KISA KIFUPI CHENYE HEKMA, MAFUNZO NA MAZINGATIO.

  Alitoka mfalme mmoja hapo zamani akiwa na waziri wake wakaenda kutembea mahali ili kujua watu wao wanahitaji nini hasa au wana kero gani ambazo wangeweza kuwaambia pasina kujua kama wao ni viongozi kwahiyo walivalia mavazi ya kawaida tu ambayo mtu yeyote yule angeweza kuwa nayo, basi wakafika katika nyumba moja na baada ya kukaribishwa alionekana mzee wa makamo ambae aliwapatia maziwa kisha wakapiga story mbili tatu na ulipofika muda wanataka kuondoka ikabidi mfalme amuulize yule mzee kwamba una lolote la kutuhusia sisi tunataka kuondoka.

Mzee akamwambia, nna vitu vitatu tu vya kukuhusia, cha kwanza kabisa usiwaamini sana viongozi hata kama wakakupenda mpaka wakakupa cheo, cha pili usiwaamini sana wake zako hata kama wakakupenda mpaka wakawa wanakuabudu wewe badala ya MUNGU, cha tatu ndugu zako watabaki kuwa ndugu zako tu hata kama ikawaje.
Basi wakaondoka lakini mfalme aliyapuuza maneno haya na kuyaona hayana maana lakini waziri akataka amuhakikishie kwamba yale maneno yana ukweli ndani yake.
Siku moja waziri akaenda kwenye bustani ya mfalme akamuiba ndege mmoja mfano wa KASUKU ambae mfalme alikuwa akimpenda sana kisha akampelekea mke wake na kumwambia amfiche tena iwe siri mtu yeyote asijue.
Baada ya siku mbili akamwambia mke wake ampe mkufu wake wa shingoni ili akauongezee vito vya thamani uwe unang'aa zaidi, basi ikapita siku ya kwanza, ya pili mke wake akamuuliza vipi mbona mkufu wangu hukunirudishia, lakini waziri akakaa kimya, zikapita tena siku zingine mke akamuuliza akakaa kimya, basi yule mwanamke kwa hasira ikabidi ampelekee mfalme yule ndege akamwambia huyu ndege ulikuwa ukimtafuta mume wangu ndo alikuja akamuiba kwenye bustani yako akamleta nyumbani na kuniambia nimfiche alafu iwe siri mtu yeyote asijue.
Basi mfalme nae kwa hasira akaita ASKARI wake na kuwaamuru wamkamate waziri kisha aletwe mbele ya watu wote kwa ajili ya adhabu yake ambayo ilikuwa ni KUNYONGWA mpaka KUFA.
Lakini kabla ya zoezi hilo aliongea nae kwa mara ya mwisho akamwambia nilikuamini sana ndugu yangu mpaka nikakuteua uwe msaidizi wangu lakini kwa hili sina msamaha na wewe.
Waziri akaongozwa mpaka kwenye kitanzi hali ya kuwa UMMA wote ukishuhudia kuangamia kwake, aliwaangalia wake zake wote wametulia tuli, akawaangalia rafiki zake pengine wangemstili, wajumbe wa baraza lake nyuso zikanawiri, zilisikika kelele za vilio kutoka kwa BABA na MAMAAKE wakimuomba mfalme ayanusuru maisha ya mtoto wao walau kwa uchache lakini ilishindikana, ikabidi BABA ajitolee KUNYONGWA yeye badala ya mwanae lakini hapa ulitamba ule msemo wa kwamba YA KAISARI muachie KAISARI.
Waziri akapewa nafasi ya kuongea mara ya mwisho ndipo akasema kumwambia mfalme unakumbuka yale maneno aliyowahi kukuhusia yule mzee kwenye kitongoji.
Alikwambia kwamba usiwaamini sana viongozi hata kama wakakupenda mpaka wakakupa cheo, angalia leo hii mimi ni waziri wako na ulinipa mwenyewe madaraka lakini unataka kuniangamiza eti kwa sababu ya ndege KASUKU tu, hilo la kwanza la pili alikwambia usiwaamini sana wake zako hata kama wakakupenda mpaka wakawa wanakuabudu wewe badala ya MUNGU, angalia leo hii mke wangu pamoja na kunipenda kote kule lakini leo mwenyewe ndiyo amekuwa sababu ya kuangamia kwangu eti kisa sikumrudishia mkufu wake tu, la tatu alikwambia kwamba ndugu zako watabaki kuwa ndugu zako tu hata kama kikatokea nini, angalia leo hii watu wote wamekaa pembeni wakisubiria niangamie lakini wazazi wangu pekee ndiyo wanajitahidi kunipambania wakiona watanisaidiaje.
Mfalme alikata tamaa pale pale baada ya kuyasikia haya na ndiyo ikawa salama ya WAZIRI.

Comments